TUKUJUZE MEDIA

TUKUJUZE MEDIA
TUKUJUZE ONLINE MEDIA

Breaking News

Dk. Shein ateta na msajili vyama vya siasa.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa Tanzania ili weze kutekeleza vyema majukumu yake katika kuimarisha demokrasia nchini.
Dk. Shein aliyasema hayo jana alipokuwa na mazungumzo na Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa Tanzania Mohammed Ali Ahmed aliyefika Ikulu mjini Zanzibar kwa ajili ya kujitambulisha akiwa amefuatana na Msajili wa Vyama vya Siasa Tanzania, Jaji Francis Mutungi.
Katika maelezo yake Dk. alisema serikali inatambua umuhimu wa ofisi hiyo pamoja na uongozi wake kwa taifa, hivyo kuna kila sababu ya kutoa ushirikiano wake kwa lengo la kuimarisha demokrasia.
Alimpongeza Naibu Msajili huyo wa Vyama vya Siasa kwa kuteuliwa nafasi hiyo na kueleza matumaini yake makubwa ya utendaji kazi wa kiongozi huyo.
Aidha, alimuhakikishia kiongozi huyo kwamba kwa upande wa Zanzibar atapewa kila aina ya msaada na ushirikiano ili aweze kufanikisha kazi zake vyema hasa ikizingatiwa kuwa ofisi yake ipo hapa Zanzibar.
Nae Jaji Francis Mutungi aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Dk. Shein kwa ushirikiano inayoyapata ofisi yake hatua ambayo imesaidia kufanikisha vyema kazi za ofisi hiyo.
Mapema Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Mohammed Ali Ahmed, alitoa shukurani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli, pamoja na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein kwa kuteuliwa kushika wadhifa huo ambao aliahidi kuutumikia vyema.
 Zanzibarleo.

Hakuna maoni