TUKUJUZE MEDIA

TUKUJUZE MEDIA
TUKUJUZE ONLINE MEDIA

Breaking News

SMZ yazidi kuimarisha huduma za kijamii, kiuchumi.

KATIKA kuimarisha huduma bora za makaazi na kibiashara Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, chini ya uongozi wa Rais Dk. Shein imekuwa ikichukua juhudi za makusudi katika kuhakikisha mambo hayo yanakaa sawa.
Hivyo, basi Serikali kupitia mfuko wa hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) imejenga nyumba bora za makaazi kwa wananchi yakiwemo maeneo ya biashara, ofisi za Serikali, na hata viwanja vya kufurahishia watoto.
Hivi karibuni, Rais Dk. Ali Mohamed Shein alilifungua jengo la nyumba ya ‘Chawl’ ambalo limefanyia ukarabati mkubwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Nyumba hiyo iliyopewa jina la ‘Chawl’ hapo mwanzo lakini watu wa Zanzibar wakaiita ‘jumba la treni’ kutokana na umbile la jumba lenyewe ambalo muonekano wao ni mithili ya treni.
‘Chawl building’ kwa lugha ya Kiingereza maana yake nyumba ya ‘Chawl’ ambapo neno ‘Chawl’ linatokana na moja kati ya lugha za Kihindi inayoitwa Marati (Marathi) ambayo inazungumzwa na takriban watu milioni 68 wa Mashariki ya India.
Kwa mujibu wa lugha hiyo neno ‘Chawl’ linahusika zaidi na staili ya ujenzi wa jengo lenyewe ikiwemo umbile lake ambapo kumbukumbu zinaonesha kuwa majengo ya staili hiyo yaani ‘Chawl’ yalianza kujengwa huko India mwishoni mwa karne ya 18 kuingia ya 19.
Aghalabu majengo hayo huwa marefu yanayofikia ghorofa 4 mpaka 5 na yalijengwa kwa madhumuni ya kuwakodisha watu kwa ajili ya makaazi hasa kwa zile familia za wafanyakazi waliokuwa na kipato cha chini, ambapo kwa wakati huo familia hizo zililipa kodi iliyokuwa ya gharama nafuu tena kwa wakati.
Nyumba ya ‘Chawl’ ambalo Shirika la UNESCO wanalitambua kama ni jengo la zamani ‘grade A’ lilijengwa katika miaka ya 1880 na mtawala wa Kisultani wa Zanzibar aliyeitwa Barghash bin Said ambapo pia, Sultani huyu alijenga majengo mengine ikiwemo Beit el Ajaib, Ikulu zake zilizokuwepo Chukwani, Maruhubi na Chuini hapa Unguja ambayo hivi sasa ni majengo ya kihistoria.
Wakati wa utawala wa Barghash jengo hilo lilijengwa kwa dhamira ya kuwa chanzo cha kuzalisha mapato katika kuanzisha na kuendeleza mradi wa maji safi na salama ndani ya mji wa Zanzibar ambapo kabla ya mradi huo inasemekana watu wakipata maji kwenye visima vidogo vidogo ambavyo maji yake hayakuwa salama kwa matumizi ya afya za binaadamu.
Kodi zilizokusanywa kutokana na jumba hilo ndizo zilizokamilisha miundombinu ya maji safi na salama katika mji mkuu wa Zanzibar lakini miundombinu hiyo haikutosheleza kusambaza maji kwa mahitaji ya sehemu zote za Unguja.
Jengo hilo ambalo lipo katika eneo la mjini Darajani ni eneo lenye harakati nyingi za kibiashara tangu kale na dahari ambapo historia ya eneo hilo imeeleza kwamba sehemu kubwa ya eneo hilo la Darajani lilikuwa ni bahari iliyotenganisha sehemu ya mjini na ng’ambo.
Ili kurahisisha mawasiliano baina ya mjini na ng’ambo lilijengwa daraja la mbao katika eneo hilo lililowawezesha watu kuvuka katika kuendesha shughuli zao na ndipo jina la Darajani likabuniwa.
Baadae sehemu ya bahari ilifukiwa na kupatikana ardhi ambayo ilitumika kwa shughuli mbali mbali za biashara, usafiri na usafirishaji, biashara na soko kubwa ambayo hadi hivi leo vinatumika.
Serikali ya Mpinduzi ya Zanzibar kwa kufahamu vizuri umuhimu wa jumba hilo la treni ililitaifisha mnamo mwaka 1964 mara baada ya Mapinduzi Matukufu na kuliweka chini ya Wizara inayohusika na nyumba katika Idara ya Mamlaka ya Mji Mkongwe na likaendelea kutumika kwa shughuli zake zile zile.
Jengo hilo lilijengwa kwa kutumia boriti, mawe, udongo na chokaa ambalo lilikuwa karibu na daraja lililounganisha sehemu mbili kutokana na kupitiwa na zaidi ya miaka 100 jengo hilo lilianza kuchakaa.
Hata hivyo, kutokana na umuhimu wake kijamii, kitalii na taswira yake katika Mji Mkongwe Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati ilikabidhi kwa Mfuko wa Jamii Zanzibar jengo hilo mnamo mwezi Juni 2016 ili kulifanyia matengengezo.
Kazi ya matengenezo ya jumba la treni ilianza rasmi tarehe 2 Novemba 2016 baada ya mkandarasi kukabidhiwa jengo hilo ambapo kazi za mwanzo zilizofanyika ni kuliongezea umadhubuti jengo lenyewe wka kulihami lisije likaanguka au kuleta madhara kabla na wakati wa ujenzi.
Hata hivyo, kutokana na uchakavu wa jengo lenyewe ilibidi Serikali itafute njia ya kulifanyia matengenezo kabla halijaathiri maisha ya wananchi.
Matengenezo na marekebisho yaliyofanywa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika jengo hilo yalikuwa na dhamira ile ile ya kwua chanzo cha mapato ambayo yatachangia katika kuendeshea shughuli nyingine za maendeleo kwa manufaa ya wananchi na nchi kwa jumla.
Hivyo, matumizi ya jengo hilo hivi sasa ni fursa nyengine kwa wafanyabiashara watakaobahatika kupata nafasi kujipatia maeneo mazuri ya kufanya shughuli zao na kuchangia kuongeza mapato ya Serikali.
Matengenezo ya jumba hilo ni miongoni mwa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015 ambayo ni kuwatengenezea wananachi maakazi mazuri kama hayo.
Pia, ni kuwawekea mazingira mazuri wananchi ya kuendesha shughuli zao binafsi za kazi za kujitafutia riziki halali.
Akifungua jengo hilo hivi karibuni, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein aliutaka uongozi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) kufanya kazi kwa uadilifu kwa kuyatekeleza maagizo ya Serikali katika ukodishaji nafasi za kufanyia biashara katika jengo la Jumba la Treni “Chawl” lililofanyiwa ukarabati mkubwa.
Katika maelezo yake Rais Dk. Shein aliutaka uongozi huo wa (ZSSF) kuwa wawazi, wasiwe na muhali na wala wasimpendelee mtu yeyote katika ukodishwaji wa nafasi za kufanyia biashara katika jumba hilo la maduka
Rais Dk. Shein pia, alisisitiza haja kwa uongozi huo wa (ZSSF) kutofanya biashara kirafiki wala kujuana kwani biashara ni heshima, hivyo ni vyema wakafanya biashara kwa lengo la kupata faida.
Aliongeza kuwa ni vyema watu wote wakazingatia kuwa nafasi na fursa zilizopo katika jengo hilo ni chache na kwa hivyo, haitowezekana kila mtu anayehitaji apewe sehemu ya kufanyia shughuli zake katika jengo hilo.
Alieleza matumaini ya Serikali kuwa kukamilika kwa mradi wa matengenezo ya nyumba ya treni kutachochea kasi ya ukuaji wa shughuli za biashara katika mji wa Zanzibar.
Dk. Shein aliwashangaa wale wote wanaokasirika na kununa wakati Serikali ikifanya mambo mazuri kwani lazima Serikali itekeleze mambo yake ikiwa ni pamoja na kujenga miundombinu yake ya kihistoria kwa madhumuni ya kuienzi historia ya Zanzibar.
Aidha, Rais Dk. Shein alieleza kuwa kuna baadhi ya miji mikubwa ulimwenguni nje ya Afrika, ambayo inasifika kwa usafi ukiwemo mji wa Singapore, Honolulu, Copenhagen, London, Geneva, Stockholm na mengineyo, hivyo ni vyema na mji wa Zanzibar ukafuata mkondo huo.
Alieleza kuwa hivyo, ni jambo la busara sana na Zanzibar ikaiga tabia ya kuvitunza vitu vyake katika hali zote ikiwemo usafi ili maeneo yake nayo yasifike kwa kuwa na mazingira safi yanayovutia.
Alisisitiza suala la usafi kwa miji yote ya Unguja na Pemba na kueleza haja ya jengo hilo ya kulitunza na kuliweka katika hali ya usafi ili lizidi kudumu kwa miaka mengine 200 ijayo.
Kuhusu ujenzi wa maduka ya kisasa katika eneo la Darajani kwenye mradi uliopewa jina la “Darajani Corridor”, Dk. Shein alieleza kuwa inayochelewesha sio Serikali bali ni Shirika la UNESCO kutokana na taratibu za Mamlaka ya Miji Mikongwe duniani lakini alieleza kuwa hata hivyo wapo baadhi ya watu kutoka Zanzibar ambao walipeleka fitna juu ya ujenzi wa sehemu hiyo huko UNESCO.
Dk. Shein alieleza kuwa hata hivyo, ujenzi wake upo pale pale ambapo mradi huo utatekelezwa baada ya kupokea maoni ya UNESCO ambayo yanategemewa yataletwa baada ya Serikali kuwasilisha kwao maelekezo waliyoyatoa takriban miaezi sita iliyopita na kueleza matarajio yake juu ya ujenzi huo kuanza mara tu baada ya kukamilika mipango hiyo, hivyo aliwataka wananchi kuendelea kuwa wavumilivu na lolote litakalokuwa watajuulishwa.
Kwa upande wa Skuli ya Darajani, Dk. Shein alisema kuwa skuli hiyo haitovunjwa kama wanavyoeleza watu wasiojua ukweli na badala yake jengo hilo litatumika kwa ajili ya matumizi mengine na wanafunzi wake watahamishiwa katika skuli mpya inayojengwa huko Rahaleo pamoja na wale wa skuli ya Vikokotoni ambao jengo lao hilo la skuli litavunjwa kwani halimo katika historia ama Mamlaka ya Mji Mkongwe na wao pia, watahamia Rahaleo.
Akieleza kuhusu ujenzi wa maduka makubwa “Shopping Malls” katika eneo la Michenzani nao upo pale pale ambapo Taasisi ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (ZSSF) ndio utakaojenga maduka hayo ambapo ujenzi wake hauna muda mrefu utaanza.
Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuwashukuru na kuwapongeza wananchi kwa kustahamili wakati wote wa ujenzi wakiwemo wale wote waliokuwa wakiishi na kufanya biashara katika Jumba hilo na kuipongeza Kampuni ya ujenzi ya CRJE East Afrika, wakandarasi wasadizi, Mshaidizi Ujenzi Kampuni ya CONS Africa na wengineo.
Aliipongeza (ZSSF), Bodi yake kwa kuyawezesha kwa ufanisi matengenezo ya jengo hilo na kuupongeza uongozi wa Wizara ya Fedha na Mipango kwa usimamizi wao mzuri wa kuhakikisha ujenzi huo unakamilika.
Ujenzi wa Jumba hilo hadi kumalizika kwake umegharimu shilingi Bilioni 11.5 ambapo jumba hilo lina milango ya maduka ya biashara 52, sehemu 2 za ATM, eneo la kusalia kwa wanawake, nyumba 10 za kuishi, mkahawa, sehemu ya kufanyia mazoezi (Gymnaslum), sehemu za ofisi, duka la mahitaji mbali mbali ‘supermarket’.
Mradi huo pia, umezingatia uwepo wa watu wenye mahitaji maalum, hivyo umewekewa ‘ramp’ itakayowawezesha kufika katika ghorofa ya chini na pia umewekewa ‘lift’ ambayo itasaidia kuwafikisha katika ghorofa ziliozobakia.
Uwekezaji wa ukarabati wa jengo la treni ni mkubwa kwa ZSSF na kukamilika kwake unaashiria kuanza kuingiza mapato, hivyo kutokana na uchambuzi uliofanywa na wataalamu mbali mbali wakiwemowa ZSSF, mradi huu utakuwa na tija kifedha, kiuchumi na kijamii.
Kwa kuzingatia vyanzo vya mapato vilivyomo ZSSF inatarajia mradi huo utajilipa ndani ya kipindi cha miaka 10 ijayo. Aidha, Serikali kupitia vyombo vyake vya kukusanya kodi itanufaika na biashara zitakazoendeshwa na wananchi mbali mbali katika jengo hilo ambalo imezikosa kwa muda.
Taasisi za Serikali kama Shirika la Umeme, Mamlaka ya maji wataweza kunufaika na mauzo ya umeme na maji yenye kutumika katika jumla hilo pamoja na kuwa kivutio kikubwa kwa watalii kutokana na haiba ya jengo hilo.
Hivyo basi kwa wale wote watakaobahatika kupata nafasi ni vyema wakaitumia vyema fursa hiyo katika kuimarisha maisha yao.
Aidha, wahakikishe wanaitunza nyumba hiyo kwa usafi, wazingatie mikataba ya ukodishwaji na kulipa jkodi kama inavyotakiwa na kuepukana na matumizi yoyote mabaya kinyume na malengo yaliokusudiwa.
Wazee walisema ‘kitunze kidumu’, hivyo kuna umuhimu mkubwa wa matunzaji wa jengo hilo ikiwa ni pamoja na kudumisha usafi wa jengo zima ndani na nje.
Iwapo linatakiwa jengo hilo liendelee kutumika kwa muda mrefu likiwa katika ubora huo ni lazima kwanza liwekwe katika hali ya usafi jambo ambalo ni muhimu na linahitaji kuwekewa mikakati maalum.
Ipo mifano ya baadhi ya majengo yakiwemo ya Serikali ambayo yamejengwa kwa gharama kubwa lakini yamepoteza haiba yake nzuri kwa kukosa mipango ya utunzaji hivyo, ni vyema jitihada zikafanyika katika kuondokana na mwenendo wa aina hiyo ili kuilinda taswira nzuri ya majengo hayo sambamba na kuzithamini gharama zilizotumika katika kuyatengeneza.
Jengo la ‘Chawl’ lipo katika kitovu cha mji wa Zanzibar ambapo kwa mnasaba huo jengo hilo linachangia katika kuupa haiba nzuri mji wa Zanzibar hasa kwa wageni wanaitembelea Zanzibar.
Ni wazi kwamba sura ya sasa ya nyumba hiyo bada ya kuifanyia matengenezo inatoa taswira njema na ya kuvutia kwa kila mtu.
Hata hivyo, kwa sababu jengo hilo limo ndani ya Mji Mkongwe ambao ni mji wenye historia kubwa ya visiwa vya Zanzibar na watu wake, bila ya shaka nyumba hiyo itakuwa inachangia sehemu muhimu ya historia ya Mji Mkongwe.
 Zanzibarleo.

Hakuna maoni